04/06/2026
ZIC YASHIRIKI JUKWAA LA UWEKEZAJI ZANZIBAR
Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) limeshiriki katika Jukwaa la Uwekezaji Zanzibar 2026 (Zanzibar Investment Summit 2026), lililofunguliwa rasmi leo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika Hoteli ya Golden Tulip Airport, Zanzibar.
Jukwaa hilo la siku tatu limewakutanisha wawekezaji, taasisi za umma na binafsi pamoja na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa lengo la kupanua fursa za biashara na uwekezaji katika visiwa vya Zanzibar.
Ushiriki wa ZIC katika jukwaa hilo unaonesha dhamira ya dhati ya kuendelea kuwa mshirika muhimu katika kukuza mazingira salama ya uwekezaji kupitia huduma mbalimbali za bima zinazolinda mali, biashara na miradi ya uwekezaji dhidi ya majanga yasiyotarajiwa.
Katika miaka ya hivi karibuni, Zanzibar imeendelea kujijengea sifa k**a moja ya maeneo yenye mazingira rafiki ya uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki, hali iliyowezesha kuvutia zaidi ya miradi 800 ya uwekezaji yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 9.
Mafanikio hayo yamechangiwa na sera na mageuzi mbalimbali ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kuimarika kwa huduma za bima zinazowapa wawekezaji uhakika na ulinzi wa shughuli zao za kiuchumi.
Kupitia maonesho ya huduma yanayokwenda sambamba na jukwaa hilo, ZIC imepata fursa ya kukutana na wadau wa uwekezaji na kuwapa elimu ya juu ya huduma zinazopatikana ZIC.
đź“… 04 Juni, 2026
📍 Golden Tulip Airport, Zanzibar