12/08/2026
Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCU) kimeendelea kuimarisha uwezo wa wanataaluma wake katika matumizi ya Akili Bandia (Artificial Intelligence – AI), utafiti, uandishi wa machapisho ya kitaaluma na utambuzi wa fursa za kitaaluma kupitia Academic Research Mentorship Clinic iliyofanyika katika Tovin Hall.
Kliniki hiyo, iliyoandaliwa chini ya RUCU Academic Staff Association (RUCU-ASA), iliwakutanisha wanataaluma wa RUCU kwa lengo la kuwajengea uwezo katika matumizi ya AI k**a nyenzo ya kuboresha ufundishaji, utafiti, uandishi wa mapendekezo ya miradi na ruzuku, pamoja na uchapishaji wa kazi za kitaaluma.
Akizungumza katika ufunguzi wa kliniki hiyo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma (DVCAA) alisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wanataaluma kuendana na maendeleo ya teknolojia na kutumia fursa zinazotokana na AI katika kuboresha elimu, utafiti na ubunifu.
Kliniki hiyo ilijikita katika maeneo mbalimbali, yakiwemo utafiti shirikishi wa fani mbalimbali (interdisciplinary research), uandishi wa maombi ya ruzuku, utambuzi wa fursa za ufadhili wa utafiti, pamoja na matumizi ya zana za AI katika kuandaa na kuboresha kazi za kitaaluma.
Mwezeshaji wa kliniki hiyo, Bw. Musa Simon kutoka Johannes Kepler University, Austria, aliwaongoza washiriki katika mada ya AI in Interdisciplinary Research and Grant Writing, akieleza namna AI inavyoweza kutumika kwa ufanisi katika utafiti, uandishi wa proposals na kutafuta fursa za ufadhili.
Aidha, washiriki walipata fursa ya kufanya mazoezi ya vitendo katika kutumia AI kuendeleza mawazo ya utafiti, kuboresha proposals na manuscripts, pamoja na kuandaa maandiko kwa ajili ya uchapishaji katika majarida ya kitaaluma.
Kliniki hiyo pia ilihusisha mada ya Research Writing and Publication, iliyolenga kuwawezesha wanataaluma kuboresha ubora wa maandiko yao na kuongeza uwezo wa kuchapisha katika majarida yenye viwango na athari kubwa (high-impact journals).
RUCU inaamini kuwa AI si mbadala wa mwanataaluma, bali ni nyenzo muhimu ya kuongeza ufanisi, ubunifu na tija inapaswa kutumiwa kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji.