02/06/2016
TAMKO LA KULAANI WIMBI LA MAUAJI YANAYOENDELEA NCHINI
Kampeni ya Vitabu na Midahalo (KVM) imesikitishwa na inalaani vikali wimbi la mauaji ya watu wasio na hatia yanayoendelea kutokea nchini. Wimbi hilo linajumuisha pia mauaji yaliyotokea katika kitongoji cha Mabatini, kata ya Mzizima, wilaya ya Tanga usiku wa kuamkia tarehe 31 Mei, 2016 na kwamba katika tukio hilo, jumla ya watu wanane wakiwemo watatu wa familia moja waliuawa kikatili.
Mauaji hayo ya Tanga, yamefanyika huku takriban watu 10 wakiripotiwa kuuawa kikatili wiki chache zilizopita katika maeneo mbalimbali wakiwemo watatu waliokuwa msikitini Jijini Mwanza.
Ikumbukwe kuwa tarehe 10 Mei, 2016 saa saba usiku, watu saba wa familia moja waliuawa kikatili katika kijiji cha Sima wilayani Sengerema na kwamba tarehe 25 Mei, 2016 saa saba usiku, mtumishi wa Wizara ya Fedha aliuawa kikatili nyumbani kwake maeneo ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Vitendo vya mauaji hayo ya kikatili vinavunja haki ya kuishi ambayo ndiyo msingi wa haki zote za binadamu. Wimbi hili la mauaji licha ya kuleta simanzi, limeibua hofu na taharuki kubwa katika jamii. Wanaopoteza maisha in ndugu zetu na watanzania wenzetu.
Kampeni ya Vitabu na Midahalo (KVM), inatumia fursa hii kutoa wito kwa Serikali kuchukua hatua za makusudi za kuwasaka wote wanaohusika na mauaji hayo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Kila mtanzania anapaswa kuwa askari wa mwenzake na kuendelea kuripoti viashiria vyovyote vya uhalifu kwenye sehemu anayoishi.
Kadhalika KVM inawaomba watanzania wrote kutambua kuwa, nchi yetu inao maadui wengi wakiwemo wa ndani na wa nje wanaopenda kuona taifa letu likisambaratika. Ni jukumu la kila mtanzania kulinda na kudumisha usalama na amani ya nchi yetu. Wote wanaojaribu kuvuruga usalama na amani ya Taifa watashindwa na kuaibika. Kwa ulinzi wa mwenyezi Mungu na kwa misingi ya umoja na mshikamano iliyowekwa na waasisi wa Taifa, Tanzania itaendelea kuwa kisiwa cha Amani kwenye mipaka ya dunia. Chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli, utangamano wa kisiasa na kiuchumi utazidi kuimarika na kamwe taifa letu halitateteleka.
Kwa upande mwingine, KVM inatoa wito maalum kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuchukua hatua za tahadhari za kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao. Suala la ulinzi na usalama iwe Agenda ya Kudumu. Wakati sasa umefika wa kurejesha na kuhuisha mfumo wa mabalozi wa nyumba kumi uliotumika miaka ya sabini enzi za Mwongozo wa TANU wa 1970.
Kuanzia sasa mabalozi wa nyumba kumi kwa kushirikiana na viongozi wa vitongoji, vijiji na mitaa wanapaswa kuwa na orodha kamili ya wenyeji na wageni kwenye maeneo yao. Kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, wahalifu watakamatwa mapema kabla hawajatekeleza vitendo vyao vya uhalifu.
Kadhalika, Wakuu hao wa Mikoa na Wilaya ambao pia ni wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama kwenye maeneo yao, wanapaswa kuanzisha utaratibu endelevu utakaowashirikisha wananchi wote kupitia mikutano ya hadhara, kuwapigia kura za siri wote wanaoshukiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Baada ya kura hizo za siri kupigwa, vyombo vya ulinzi na usalama vitafanya uchunguzi wa kina ili kujiridhisha na uhalali wa kura hizo. Zaidi ya hayo, KVM inaishauri Serikali kuanzisha Mfumo wa Utoaji wa Tahadhari Mapema ( Early Warning System) na kwamba, mfumo huo kwa upande mmoja, utawashirikisha wananchi na kwa upande wa pili, utashirikisha vyombo vya ulinzi na usalama.
Lengo la mfumo huo, litakuwa ni kubaini viashiria vya uhalifu na kudhibiti vitendo vya uhalifu kabla havijatokea pamoja na kuwakamata wahalifu wenyewe. Ni vizuri hatua hiyo iende sambamba na utoaji wa elimu ya uzalendo na uraia kwa watanzania wote. Kadhalika, Serikali inaweza pia kuangalia uwezekano wa kupanua zaidi mafunzo ya mgambo na JKT kwa vijana kwa lengo la kuweka mshikamano wa nadharia na vitendo kuhusu suala la ulinzi na usalama wa nchi yetu.
Mungu ibariki Afrika.
Mungu ibariki Tanzania!