23/02/2016
NIDHAMU KATIKA MALENGO
Kila mmoja ana malengo juu ya kile anahitaji kukamilisha ndani ya muda fulani katika maisha yake. Kuna idadi fulani ya watu pia hawana kabisa malengo waliyojiwekea ndani ya muda fulani, jambo hili ni hatari katika kuboresha maisha.
Utafiti unaonesha idadi ya watu wengi huwa hawafikii malengo waliyojiwekea, na wengine huyatupilia mbali katika hatua za mwanzo tu za utekelezaji. Sababu moja wapo inayochangia kukwamisha ni NIDHAMU katika malengo yao.
Je ? Unaheshimu malengo yako wakati wowote kuanzia unaamka hadi unaenda kulala? Je? Uko tayari kusema hapana kwa jambo ambalo ni kinyume na malengo yako? Uko tayari kusimama kutetea malengo yako pale unapokutana na vikwazo? Unatumia muda kiasi gani kutekeleza malengo yako?
Waweza ukawa na kila aina ya rasilimali k**a vile elimu , pesa, nguvu kazi na nyingine nyingi lakini ukajikuta unashindwa kufanikisha kile ulichokusudia. Wakati mwingine ni NIDHAMU ya utekelezaji pekee ndio inayokukwamisha. Leo unanza kesho unaacha, kesho kutwa unaanza tena siku ijayo unaacha, unakosa nidhamu.
Unapoweka malengo hakikisha unakuwa na nidhamu katika utekelezaji wake, heshimu malengo yako, kuwa tayari kuyapigania na kuyatetea wakati wote, jitoe mzima mzima kwa ajili ya malengo hayo na siku zote yawe ndio kipaumbele katika mawazo na matendo yako.
Na.....Vicent Stephen